News

Posted date: 19-May-2024

TANESCO visited TGDC

News Images

Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania TANESCO wakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga Mei 18, 2024 wamefanya ziara ya kikazi kutembelea na kuzungumza na menejiment pamoja na wafanyakazi wa Kampuni yake tanzu ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania TGDC kwa lengo la kujenga ari ya kazi pamoja na kujua hatua mbalimbali za maendeleo ya miradi inayotekelezwa na kampuni yake hiyo.

Akiongea baada ya kupata taarifa fupi ya utekelezaji kutoka TGDC, Mkurugenzi Mkuu TANESCO Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga amesema, lengo la ziara hiyo ni kuikutanisha menejimenti ya TANESCO na TGDC ili kuweza kuzungumza na kujua mafanikio pamoja na changamoto zinazoikabili kampuni ili mwisho wa siku, lengo la kuzalisha umeme wa jotoardhi litimie huku akisisitiza kuwa TGDC inafanya kazi nzuri.

“niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninajua kuwa mnatamani sana nanyi muanze kuzalisha umeme, mtazalisha ninaamini. Kikubwa kwenu niombe muendelee kuwa wabunifu na kutumia teknolojia rahisi kutokana na kujifunza kwa wengine ili Tanzania tutumie muda mfupi kuliko waliotangulia katika upatikanaji wa nishati hii jadidifu”, alisema Mhandisi Nyamo-Hanga.

Mhandisi Nyamo-Hanga ameongeza kuwa, “TANESCO na TGDC ina jukumu la kupanga pamoja kwani ikifanikiwa TANESCO imefanikiwa TGDC na ikifanikiwa TGDC imefanikiwa TANESCO hivyo ushirikiano baina yetu ni wa muhimu sana”

Alimaliza kwa kuahidi kuendelea kuhakikisha TGDC inafanikiwa kwa kila jambo ikiwemo kufanikisha maandalizi ya Kongamano kubwa la Jotoardhi katika Ukanda wa Afrika ARGe0-C10 litakalofanyika nchini kuanzia tarehe 21-27 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa kimataifa wa mwl.Julius Nyerere uliopo jijini Dar es Salaam.

Kwa nyakati tofauti, wajumbe wa Menejimenti ya TANESCO walisema, wako tayari na wataendelea kutoa ushirikiano kwa TGDC na kwamba Watanzania wana kiu ya kuiona nishati ya Jotoardhi ikitoka, hivyo ni muhimu kuendelea kushikamana kufanikisha upatikaji wake.

Akitoa taarifa ya utekelezaji, meneja mkuu wa kampuni ya uendelezaji jotoardhi Tanzania TGDC mhandisi Mathew Mwangomba amesema, “tunatambua kuwa umeme ni uchumi, umeme ni burudani na umeme ni usalama, na ndio maana tunadaiana megawati moja kwa kila mtumishi. Kwa kutambua mabadiliko ya tabia nchi, TGDC pia ni mkombozi wa mazingira kwani nishati hii ni safi na ni rafiki wa mazingira. Tuna ahidi, umeme tutaupata nasi tuchangie kwenye gridi ya taifa kuweka uimara wa upatikanaji wa nishati ya umeme”

Mhandisi Mwangomba alimaliza kwa kuishukuru Serikali kwa ujumla kupitia TANESCO kwa kuendelea kuiwezesha kutekeleza majukumu yake na kwamba maelekezo yote yaliyotolewa na mkurugenzi mkuu TANESCO yatazingatiwa na kutekelezwa na watumishi wa TGDC.