News

Posted date: 07-Jun-2024

Mbeya Expo 2024 Yahitimishwa, Wananchi Wanufaika na Elimu ya Jotoardhi

News Images

Maonesho ya Pili ya Mbeya City Expo 2024 yaliyodumu kwa siku nane kuanzia tarehe 23 Mei, 2024 yamehitimishwa Mei 30, 2024 na mkuu wa wilaya ya Mbeya Mheshimiwa Beno Malisa huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamli kwakuwa wanao mchango mkubwa katika kuinua uchumi.

Ameyasema hayo wakati akihutubia wakazi wa Mbeya baada ya kupita na kutembelea mabanda mbalimbali likiwemo banda la Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania TGDC na kupongeza uwekezaji uliofanywa na unaoendelea kufanywa na serikali ili kuhakikisha Nchi inakuwa na vyanzo mchanganyiko vya nishati safi ikiwemo jadidifu ya jotoardhi.

TGDC ikiwa miongoni mwa washiriki wa maonesho hayo, iliyatumia vyema kuelimisha wananchi na wadau mbalimbali juu ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi ambapo ilileta hamasa kubwa kwa wadau ambao hawakuwa wanafahamu jotoardhi inaweza kuzalisha umeme kwa kutumia mvuke wake.

Akiongea kwa shauku baada ya kupata maelezo juu ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi, mmoja wa watembeleaji maonesho aliyefika kwenye banda la TGDC mzee Lukomano Msokwa ambaye ni mkazi wa Mbeya alisema, “kwakweli nimeshangaa na nimefurahi sana kujua kumbe tunaweza kuzalisha umeme kupitia mvuke wa jotoardhi. Hakika Mungu ameibariki Tanzania, na hakika niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa ya kuja na wazo hili hakika nchi itafurahia nishati safi kwa kiwango kikubwa sana”

TGDC inaendelea kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na Shirika mama TANESCO kwa jinsi inavyowekeza rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kuwezesha ufanikishaji wa upatikanaji wa rasilimali hii adhimu ya jotoardhi kwa maendeleo ya taifa la Tanzania.