News

Posted date: 28-Mar-2023

Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania ilivyosherekea siku ya wanawake Duniani.

News Images

Wanawake dunia nzima mwezi machi kila mwaka wana siku yao muhimu ya kushehereka siku ya Wanawake Duniani. Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania TGDC nayo haikubaki nyuma katika siku hii adhimu kwani waliungana na wanawake wengine katika maandamano ya kusheherekea siku hiyo iliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam.

Akizungumza kwa niaba yao katika tafrija fupi iliyofanyika katika ofisi za TGDC Makao Makuu, Msasani Jijini Dar es salaam, Meneja Rasilimaliwatu na utawala wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania bi, Judith Gowelle amewataka wanawake wote kutoka katika kampuni hii kuwa chachu ya mabadiliko kwa kufanya kazi kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu ili rasilimali hii adhimu ya jotoardhi ije kuwa kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Sisi kama wanawake kutoka Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania Makao Makuu na tunaungana na Bodi yetu ya Wakurugenzi kupitia kwa Meneja Mkuu Mhandisi Mathew Mwangomba ,kwenye mapinduzi makubwa ya uchumi wa nchi kwa kuhakikisha mchango wetu unakuwa mkubwa kwenye ukuaji wa rasilimali hii kwa kutumia nafasi tunazotumikia kwa kuaminiwa na viongozi wetu kwani uwezo tunao na nia pia tunayo,” amesema bi Gowelle.

Katika hatua nyingine Kaimu Meneja Mkuu Mhandisi Jasson J. Katule wakati anamkaribisha Mgeni Rasmi Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa TGDC Wakili Lucy Sondo amewataka wanafunzi wa kike nchini kusomea masomo ya sayansi, uhandisi, Sheria na kujiamini ili kuongeza mchango kwenye Sekta ya Nishati hasa masuala ya Jotoardhi.

Katika hatua nyingine amepongeza uongozi wa TGDC kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa wanawake kipaumbele kwenye utendaji kazi na kupelekea wao kuendelea kujiamini kwa kujiona ni wa thamani.

Kwa upande wa Mgeni rasmi ambaye ni Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi wa TGDC wakili, Lucy Sondo amewataka wanawake wote kwanza kujikomboa kifikra na hasa TGDC na jamii kwa ujumla. ”Natoa salaam za pongezi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi Prof. Shubi Kaijage anaungana nanyi katika siku hii muhimu, Napenda kuwaambia ninyi ni wanawake wa shoka hivyo basi fanyeni kazi kwa bidi kwani Kampuni hii ya TGDC ina mategemeo makubwa sana na ninyi, msikatishwe tamaa kwa hali yoyote ile na changamoo yeyote inayokuja mbele yenu ichukulieni ni kama fursa katika kuipata rasilimali hii ya Jotoardhi”.

Alisisitiza mashikamo sehemu za kazi kwa wanawake hata wanaume. Timu yeyote inayofanikiwa ni ile ambayo inafanya kazi zake kwa umoja na ushirikiano.Katika kushughulika na teknolojia wanawake wa TGDC msibaki nyuma. Kwani humu kuna kila fani kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake ili tuitoe TGDC ilipo. Siku ya wanawake duniani kwa mwaka huu inaongozwa na kaulimbiu inayosema “ Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia.”