Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Tanzania Geothermal Development Company

(TGDC)

Salaam za Ukaribisho kutoka kwa Meneja Mkuu

Kwa niaba ya Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC) ningependa kuwajulisha uwezo wa jotoardhi uliopo nchini Tanzania kama ulivyobainishwa kwenye tovuti hii. Jotoardhi ni maliasili inayopatikana kwa wingi Tanzania, kwa kukisia kinadhariaTanzania ina zaidi ya 5000MWe ya nishati ya jotoardhi inayosubiri kuendelezwa.

Tofauti na vyanzo vya nishati nyingine jadidifu, jotoardhi ina sifa za kipekee zinazoifanya ihitajike zaidi kwenye mfumo wa nishati Tanzania; ina manufaa kimazingira na kijamii ukilinganisha na njia kuu nyingine mbadala za uzalishaji umeme zilizoko nchini. Kuanzishwa kwa TGDC, kati ya mambo mengine, kunaendana na (i) Dira ya Maendeleo Tanzania 2025 inayokusudia kuwa na taifa lenye viwanda na uchumi wa kati; (ii) Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA). (iii) Sera ya Taifa ya Nishati 2003. Uchumi unaokua kwa kasi ni lazima upate vyanzo vya nishati vilivyo endelevu na nafuu ambapo jotoardhi ni miongoni mwa nishati bora.

Kwa niaba ya wafanyakazi wa TGDC ningependa kutoa shukrani za dhati na zaidi shukrani kwa TANESCO, Wizara ya NIshati na Madini, Taasisi za Umma, Wabia wa Maendeleo, na wadau wengine waliochangia Kampuni kutimiza malengo yake.

Mwisho, tunakaribisha wapenzi na wadau wa jotoardhi kufanya kazi kwa kushirikiana na TGDC na wabia wake kufanikisha fursa zilizoainishwa katika Tovuti hii, pamoja na kukuza uwezo na kugharimia awamu za utafutaji za miradi ya jotoardhi na kuendeleza maeneo ya mvuke Tanzania.

Serikali imeweka tayari mfumo imara wa kimaendeleo wa ushirikiano na wabia mbalimbali katika jitihada mbalimbali kutoka uchunguzi, uchimbaji, kuzalisha umeme na matumizi ya moja kwa moja. Kampuni pia inahamasisha kuhusu manufaa ya jotoardhi yahusuyo jamii ya Tanzania.

Mhandisi Kato Kabaka,

Meneja Mkuu.