Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Tanzania Geothermal Development Company

(TGDC)

Utafiti

Utafutaji wa jotoardhi ni mwingiliano wa taaluma nyingi unaohusisha jiolojia, chemia ya ardhi, maumbile ya dunia, uhandisi wa hifadhi, na taaluma za haidrolojia ili kubainisha uwepo na jiometri ya rasilimali ya jotoardhi na halijoto ya hifadhi.Kwa sasa TGDC inafanya utafiti wa kina wa jotoardhi kwenye maeneo mitatu, ambayo ni:

  • Eneo la Jotoardhi Ngozi

Utafutaji wa Jotoardhi Ngozi upo Msitu wa Akiba Poroto kwenye Wilaya ya Rungwe na Mbeya Vijijini katika Mkoa wa Mbeya Kusini Magharibi mwa Tanzania. Eneo hili lipo ndani ya ‘ Quatermary Rungwe Volcanic Province’ katika makutano matatu ya Mfumo wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, ambapo tawi la mashariki na magharibi hukutana (bonde la Nyasa-kusini, bonde la Usangu-Kaskazini Mashariki, na bonde la Rukwa – Kaskazini Magharibi). Eneo hili lina koni za volkano za hivi karibuni na eneo la volkano maarufu zaidi ni Ziwa la Kaldera la Ngozi.
Huu ni mradi uliopiga hatua kubwa sana kwa utafiti wa kisayansi ardhi ambao umewahi kufanyika hadi sasa, ambapo imebainika kuwepo na uwezekano mkubwa wa uzalishaji umeme na matumizi ya moja kwa moja ya rasilimali ya jotoardhi. Uchimbaji wa uchunguzi unatarajiwa kuanza katika Mwaka wa Fedha 2016.

  • Utafutaji Jotoardhi Kisaki

Eneo la utafutaji wa jotoardhi Kisaki linapatikana ndani ya eneo tengevu la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi , Wilaya ya Morogoro Vijijini mkoani Morogoro, mashariki mwa Tanzania.Utafutaji huo umo kwenye bonde la mashapo la Bonde la Rufiji tawi la Mashariki la Mfumo wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Baada ya uchunguzi, utafiti wa kina sasa unaendelea kufungua na kuendeleza uwezo wa jotoardhi wa eneo hilo.

  • Utafutaji Jotoardhi Luhoi

Eneo la jotoardhi la Luhoi lipo Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani mashariki mwa Tanzania Bara. Eneo hilo linaangukia katika mashapo ya bonde la Rufiji kwenye mwatuko wa ‘Karoo’ unaendelea Pwani ya Mashariki ya Tanzania. Utafutaji huu unavutia zaidi kwa kuwa unaangukia kwenye eneo ambapo utafutaji wa mafuta na gesi umekwisha kufanyika na uchunguzi wa awali wa data unaonesha uwezekano wa kuweko na rasilimali ya jotoardhi katika eneo hilo.