Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Tanzania Geothermal Development Company

(TGDC)

Kuhusu Jotoardhi

Neno jotoardhi linatokana na maneno mawili: joto na ardhi. Chanzo cha joto hili ni pamoja na matokeo ya shughuli za magma zinazotokea ndani ya dunia kama milipuko ya volkano. Nishati hii ya joto hupatikana kwa kutoboa shimo linaloruhusu ufikiwaji wa vimiminika vilivyopashwa moto kuwa mvuke.
Nishati ya jotoardhi inasemwa kuwa ni nishati kijani kutokana na ukweli kwamba uendeshaji wa jotoardhi hauhusishi uunguzaji wa mafuta ya visukuku na hivyo hewa ya ukaa inayozalishwa ni kidogo.
Nishati ya jotoardhi ni moja ya chanzo cha nishati kinachopendelewa hasa kutokana na dunia hivi karibuni kujishughulisha na kuongezeka kwa joto ambapo sekta ya nishati imekuwa ikichangia kwa wingi uzalishaji wa hewa ukaa. Utumiaji wa nishati ya jotoardhi unaweza kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na hivyo kupunguza athari za joto duniani.

Matumizi na Manufaa ya Nishati ya Jotoardhi
Jotoardhi ina matumizi mengi, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme, kilimo cha bustani, kilimo, kukausha miti, ufugaji wa samaki, uondoaji vijidudu kwenye maziwa, udobi, kilimo cha nyumba za kioo za kuhifadhi mimea, utengenezaji karatasi, madhumuni ya burdani na hufaa kitabibu kwa kutuliza maumivu.
Manufaa ya jotoardhi yanahusisha, pamoja na mengine, ni jadidifu, chanzo safi cha nishati, rahisi, uhakika, ufanisi katika ubadilikaji na isioathiriwa na hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya nchi.
Nishati ya jotoardhi inatumiwa na nchi 82 duniani, zikiwemo 24 zinazozalisha umeme na 82 zikitumia moja kwa moja kwenye matumizi mengine.
Ishara za juu ya ardhi za nishati ya jotoardhi
Ishara za juu ya ardhi za jotoardhi zinahusu umbile lolote au kiashirio juu ya uso wa dunia kinachoashiria uwepo wa mfumo wa jotoardhi chini ya ardhi. Mifano ya viashirio hivyo ni chemchemi za maji moto, ufa kwenye milima ya volkano inayotoa mvuke, madimbwi ya matope yaliyobadilishwa, mashapo ya silika na mengine, majani ya jotoardhi (fimbrisylis exilis), milipuko ya volkano, lava mpya na uwepo wa kaldera.

Mfumo wa jotoardhi una maumbile manne ambayo ni: chanzo cha joto, hifadhi, mwamba wa mfuniko na eneo la kuchaji tena. Jotoardhi kutoka kwenye chanzo hupasha moto maji kwenye hifadhi; maji moto na mvuke (kutegemea na nguvu ya chanzo cha joto) husafiri kupitia mifumo ya jiolojia na kuonekana juu ya uso wa dunia.